Azimio la Kilimanjaro 2.0 – Maono yaliyosasishwa ya vuguvugu la Africans Rising
Azimio la Kilimanjaro linaelezea falsafa ya msingi ya vuguvugu la Africans Rising. Ilipitishwa kwa kauli moja katika Kongamano la Uthibitishaji la mwaka 2016 ambalo lilihudhuriwa na wajumbe 272 wa Afrika kutoka zaidi ya nchi 40 katika MS TCDC jijini Arusha, Tanzania.
Azimio hilo linawaunganisha wanachama wote wa vuguvugu la Africans Rising, kwa ajili ya Umoja, Haki, Amani na Utu, ambalo lilizinduliwa rasmi mnamo Siku ya Ukombozi wa Afrika, tarehe 25 Mei, 2017. Kama waraka wetu wa msingi, azimio hilo linaelezea imani yetu sisi sote katika kutambulika kwa utajiri wa Bara la Afrika, watu wake waliomo barani, pamoja na nje ya bara la Afrika, na vilevile kujitolea kwetu kuondokana na mifumo dhalimu inayowakandamiza Waafrika, pamoja na na watu wenye asili ya KiAfrika.
Baada ya miaka mitano ya kwanza ya mafanikio ya vuguvugu, wanachama wetu walifanya uchambuzi wa kina wa Azimio la Kilimanjaro. Kupitia mfululizo wa mashauriano ya kikanda, wanachama wa Africans Rising walitoa maoni ya kina kuhusu jinsi Azimio la Kilimanjaro linavyoweza kurekebishwa ili kuendana vyema na matakwa ya wanachama wote wa vuguvugu letu linalozidi kukua katika ulimwengu huu unaobadilika.
Kutokana na maoni hayo, usimamizi wa Africans Rising uliunda timu ya masahihisho iliyojumuisha wanachama kutoka Kongamano la awali la Uthibitishaji na wawakilishi kutoka kila eneo la bara. Timu hiyo iliongozwa na Mabalozi wetu wawili, mwanaharakati Jay Naidoo na Mheshimiwa Fatoumata Tambajang-Jallow, makamu wa rais wa zamani wa Gambia.
Baada ya siku kadhaa za majadiliano ya kina, timu ilitoa azimio jipya, Azimio la Kilimanjaro 2.0, ambalo liliwasilishwa kwa washiriki katika Kongamano la pamoja la mavuguvugu ya Kiafrika la mwaka wa 2022 (AAMA) ili kuzingatiwa na kupitishwa. Lilikubaliwa ipasavyo na kongamano tarehe 31 Agosti, 2022, jijini Arusha, Tanzania.
Azimio la Kilimanjaro 2.0 litaendelea kutumika kama mwanga wa kuiongoza harakati tunapozidi kufanya kazi kwa lengo la ukombozi wa kweli wa KiAfrika. Tunakualika ulisome azimio hili kwa ukamilifu na ulieneze kwa Waafrika, washirika na wafuasi unaowajua kuwa wamejitolea kwa maadili ya umoja wa Kiafrika (Pan-African Unity).